Part 2..Finality of Prophethood by Maudodi

Mtume Mpya ni laana na si neema kwa Umma

Nukta ya tatu, ambayo yahitaji kutiliwa, ni kuwa pale Mtume anapotumwa kwa watu fulani suwala la imani na ukafiri, mara nyingi, hujitokeza miongoni mwa watu hao. Umma wa walioamini na makafiri, hujikuta wakiunda jamii tofauti.

Tofauti inayozitenganisha jamii hizi mbili siyo nyepesi au ya juu juu bali ni tofauti ya msingi tena ya msingi kabisa kati ya kumuamini na kutomuamini Mtume; na jamii hizo mbili kamwe haziwezi kuungana isipokuwa labda watu wa upande mmoja waamuwe kuachana na imani yao.

Mbali na hivyo, jamii hizi mbili hupata muongozo na shariya zao kutoka vyanzo viwili tofauti. Kundi moja hufuwata sheriya zitokanazo na Kitabu cha MwenyeziMungu na sunna za Mtume; Jamii nyingine kimsingi hupingana na imani hii ya Mtume kuwa ndio chanzo cha sheriya.

Kwa msingi huu inakuwa muhali kwa pande hizi mbili kuungana katika jamii moja yenye mshikamano. Itadhihidhika wazi kabisa kwa mtu anayetiliya maanani mambo hayo ya juu kwamba kukamilika kwa utume ni neema kubwa ya Allah kwa Waislamu. Ni kwa sababu hii Umma umeweza kujenga undugu wa kilimwengu daimadumu.

Imani juu ya mwisho wa utume umeinusuru jamii na hatari ya mfarakano wa kimsingi ambayo matokeo yake ingeweweza kusababisha mgawanyiko wa kudumu.

Sasa basi kila mtu anayemkubali Muhammad kama kiongozi aliyeteuliwa na Mungu yumkini na asiyetafuta nasaha kutoka chanzo chochote isipokuwa ujumbe wa MwenyeziMungu aliokuja nao Mtume mtukufu basi huyo ni ndugu katika undugu wa Kiislamu. Na kwa msingi huo, anaweza kujiunga na jamii hii wakati wowote.

Kama ofisi ya Utume isingelifungwa kabisa baaada ya Muhammad Waislamu wasingeliweza kuunda jamii yenye mshikamano; kwani kila Mtume mpya angeubomowa umoja wa umma.

Mtu mwenye akili timamu, baada ya kutafakari kidogo atafikia hitimisho kuwa ikiwa Mtume ametumwa kwa walimwengu wote (na si kwa jamii au Taifa fulani tu), na ikiwa ujumbe wa Mwenyezi Mungu umefikishwa kikamilifu kupitia Mtume huyu na zaidi ya hivyo, ikiwa mafundisho ya Mtume huyu yamehifadhiwa kikamilifu, Ofisi ya Utume hapana budi ifungwe baada yake ili ulimwengu mzima uungane kumtii Mtume huyu na kujenga undugu wa jamii moja ya waumini.

Ni kwa njia hii tu ndipo udugu wa kilimwengu wa Waislamu unapoweza kunusurika dhidi ya mifarakano isiyo ya lazima ambayo ingeweza kuibuka mara kwa mara kila anapokuja Mtume mmoja baada ya mwingine.

Mtume anaweza kuwa Mtume kivuli au buruzi; au anaweza kuwa Mtume mwenye shariah na kitabu cha Mungu. Kutokea kwa yeyote kati ya Mitume hao walioteuliwa na Mungu kungelikuwa na athari ya kijamii kwa wafuasi wake wanaounda umma mmoja na wapinzani wake wangelishutumiwa kama Makafiri na ndio kusema wametoka katika Uislamu.

Mgawanyiko huo wa walimwengu hauepukiki pale ambapo hitajio la Mtume haliepukiki. Lakini pale ambapo hakuna hitajiyo hilo, ni muhali kutarajiya eti Allah Mwingi wa Hikima na Rehema, pasipo ulazima wowote asababishe mfarakano miyongoni mwa viumbe vyake juu ya suwala la Imani na kufuru, hivyo kuwazuwiya waja wake kuunda umma mmoja daima dumu.

Kwa hiyo kile kinachothibitishwa na Qur’an kile kinachothibitishwa waziwazi na Hadith pamoja na muwafaka wa Shura ya Umma, piya kinathibika kiakili. Akili inataka hivyo kwamba ofisi ya utume ibakiye imefungwa katika wakati wote ujao.

Ukweli juu ya “Masihi” yaani “mtu wa mfano wa Yesu Kristo”

Wale wanaopiga propaganda ya Utume mpya ( kwa mfano Ahmadiya/Kadiani) mara zote, huwaambiya Waislamu wa kawaida kuwa Hadith zimebashiri kuja kwa “Masihi”.

Wao wanadai kuwa Isa alishakuwa Nabii, hivyo ujiyo wake wa mara ya pili haupingani na dhana ya mwisho wa utume ( uliokomeya kwa Muhammad). Dhana ya mwisho wa utume ni dhana sahihi, lakini hata hivyo, dhana ya kuja kwa “Masihi” nayo piya ni sahihi.

Lakini wanafafanuwa zaidi kuwa “masihi” haina maana kuwa ni yule Isa mwenyewe mwana wa Mariyamu (as). Kwani Isa (as) amekufa. Mtu ambaye kuja kwake kumebashiriwa katika Hadith ni mtu wa mfano wa Masihi Isa. Na ni mtu fulani fulani ambaye tayari amekwishafika. Kumfuwata mtu huyo siyo kupingana na imani juu ya mwisho wa utume.

Ili kuuelewa urongo wa dai hili tunanukuu hapa Hadith sahihi zinazozungumziya suwala hili huku tukinukuu vyanzo sahihi vya mapokezi ya Hadith.

Baada ya kuyapitiya makusanyo ya Hadith, msomaji anaweza kukata hukumu yeye mwenyewe namna maneno ya Mtume Mtukufu yanavyoenezwa kwa maana isiyoshabihiyana na maana ya maudhui yake halisi.

Hadith zihusiyanazo na kushuka kwa Yesu

Sayidina Abu Huraira ameripoti kuwa Mtume wa Allah kasema: “Naapa kwa Yule Mwenye mamlaka juu ya uhai wangu, Mwana wa Mariyamu atashuka miyongoni mwenu kama kiongozi mwadilifu. Atavunjavunja msalaba na kuuwa nguruwe; (Taz. Tanbihi 5) na atakomesha vita”. (Bukhari, Kitab Ahdith al Anbiya; Bab:Nuzul Isa Ibn Maryam; Muslim, Bab: Bayan Nuzul Isa; Tirmidhi, Abwab-al-Fitan; Bab Fi Nuzul Isa; Musnad Ahmad, Marwiyat Abu Huraira).

Katika hadith nyingine neno jizya limechukuwa nafasi ya neno harb, “vita”, yaani atakomesha jizya kwa wasio waumini. (Taz. Tanbihi 6)

-Hadith nyingine iliyoripotiwa na Sayidina Abu Huraira inasema. “Kiyama hakitasimama kabla ya kushuka Isa mwana wa Maryamu”, na maneno haya yanafuatiwa na maneno yaliyotajwa katika Hadith hapo juu. (Bukhari, Kitab-ul-Muzalim: Bab: Kasr-ul-Salib Ibn Majah, Kitab-ul-Fitan al-Dajjal).

Sayidina Abu Huraira ameripoti kuwa Mtume wa Allah kasema: “Je ninyi mtakuwaje pale Isa mwana wa Maryamu atakaposhuka miyongoni mwenu na mtu mmoja miongoni mwenu atasimama katika nafasi ya Imam (Kiongozi wa sala) (Taz. Tanbihi 7) (Bukhari, Kitab Abadith Anbiya, Bab: Nuzul Isa; Muslim, Nuzul Isa ; Muslim, Nuzul Isa ; Musnab Ahmad, Marwiyat Abu Huraira).

Sayidina Abu Huraira amemkariri Mtume akisema: “Kisha Isa Mwana wa Maryamu, atauwa nguruwe na ataondosha msalaba. Sala ya jamaa itafanywa kwa ajili yake. Atagawanya kiyasi kikubwa mno cha mali ambapo hakuna mtu atakayebakiya katika shida ya kitu chochote. Atafuta kodi. Atapiga kambi Rauha ( mahali pa umbali wa maili 35 kutoka Madina) na kutoka huko atafanya Hija au Umra au zote mbili.” ( Muhadithiaji ana hatihati ni ibada ipi kati ya hizi mbili iliyotajwa na Mtume mtukufu. (Musnad Ahmad, Silsila Marwiyat Abi Huraira; Muslim, Kitab-ul-Hajj; bab Jawaz-ul- Tammatu fil-Hajj wa-al-Qir’an)

-Sayidina Abu Huraira amesimuliya kuwa Mtume wa Allah baada ya kuelezeya kuja kwa Dajjal akasema, Waislamu watakuwa wakijiandaa kwa vita dhidi ya Dajjal na watakuwa wanapanga safu tayari kwa sala na Iqama itakuwa imeshatolewa kwa ajili ya sala ambapo wakati huo huo, Isa (a.s), mwana wa Maryamu atashuka na atawaongoza Waislamu katika sala. Adui wa Allah, Dajjal akimuona tu (Isa) ataanza kuyeyuka kama chumvi inavyoyeyuka katika maji. Kama Isa (a.s) atamuwachiya hivyo hivyo, basi atayeyukiya mbali na kufiliya mbali, lakini Mungu atafanya Dajjal afiye mikononi mwa Isa (a.s) ambapo Isa atawaonesha Waislamu mkuki wake uliotapakaa damu ya Dajjal.” (Mishkat, Kita-ul-Fitan, Bab : al-Malahim, iliyonukuliwa na Muslim).

-Sayidina Abu Huraira ameripoti kuwa Mtume wa Allah kasema: Hakuna Mtume atakayekuja baina ya kipindi changu na cha Isa na Isa atakuja tena. Mtambuweni pale mtakapomuwona; ni mtu mwenye kimo cha kati na kati na mwenye rangi nyekundu, ... Atavaa mapande mawili ya nguwo za njano. Nywele zake za kichwani zitaonekana kama vile zinachuruzika maji, japo nywele zake hazitakuwa na maji. Atapiganiya dini ya Uislamu .Atauvunja msalaba vipande vipande. Atauwa nguruwe. Atafuta jizya kwa Makafiri. Katika zama zake Mungu ataondosha imani zote isipokuwa dini ya Uislamu. Na Isa atamuuwa Dajjal. Ataishi duniyani kwa miyaka arobaini na utakapokwisha muda huo naye atafariki duniya. Waislamu watamsaliya sala ya maiti. (Abu Dawud, Kitab-ul-Malahim, Bab : Khuruj-ul-Dajjal; Musnad Ahmad, Marwiyat Abu Huraira).

-Sayidina Jabir bin Abdullah ameripoti kuwa alimsikiya Mtume akisema: Kisha Isa mwana wa Maryamu atashuka. Imamu wa Waislamu atamwambiya, “Njoo, utusalishe”, lakini yeye atajibu, “Hapana kuweni na maimamu wenu wenyewe katika sala. (Taz. Tanbihi 8). Atasema haya kutokana na hadhi ambayo Mungu amewapa Waislamu” (Muslim, Bayan Nuzul Isa Ibn Maryam, Musnad Ahuad, Baslsila Marwiyat Jabir bin Abdullah).

 

-Kuhusiyana na Kisa cha Ibn Sayyad, Jabir bin Abdullah anasema kuwa Umar bin Khattab (r.a) kasema: “Ewe Mtume wa Allah, niruhusu nimuuwe (Ibn Sayyad). Katika kumjibu, Mtume wa Allah akasema, “Ikiwa kweli mtu huyu ni Dajjal basi atauwawa na Isa mwana wa Maryamu. Wewe hutamuuwa. Lakini kama mtu huyu si Dajjal basi huna haki ya kumuuwa mtu miongoni mwa watu ambao tumechukuwa dhamana ya kuwalinda.(Madhimi).” (Mishkat. Kitab-ul-Fitan, Bab: Qissa Ibn Sayyad, quoted by Shara al-Sunnah: Baghawi).

-Jabir b. Abdullah amesimuliya kuwa wakati akisimuliya kisa cha dajjal, Mtume mtukufu wa daraja alisema: Wakati huwo Isa bin Mariyamu atashuka ghafla miyongoni mwa Waislamu. Jamaa itaungwa kwa ajili ya sala na ataombwa: “Ewe roho wa Mungu njoo mbele utusalishe”. Lakini yeye atasema, “Hapana, Imamu wenu ndio apite mbele na kuwa msalishaji. “Hivyo pale Waislamu watakapokuwa wamesali sala ya alfajiri watatoka nje kwenda kupambana na Dajjal. Pale mdanganyifu huyo atakapomuwona Isa (as), ataanza kuyeyuka kama chumvi katika maji. Isa atamsogeleya na kumuuwa. Na itatokeya kuwa kila jiwe litaliya kwa kelele : “Roho wa Mungu huyu Yahudi kajificha nyuma yangu. “Hakuna hata mfuwasi mmoja wa Dajjal atakayeepuka kifo.” (Musnad Ahmad, Basissila Riwayat Jabir, Abdullah).

-Sayidina an-Nawas b. Sam’an (wakati akisimuliya kisa cha Dajjal) amesema: “Palepale Dajjal atakapokuwa anashughulika kuendeleza mambo hayo, Mungu atamtuma Isa, mwana wa Mariyamu. Isa (as) atashuka jirani na white Tower(Mnara Mweupe) katika eneo la mashariki la Damascus, akiwa amevaa mapande mawili ya nguwo ya manjano na mikono yake akiiweka juu ya mikono ya malaika wawili. Pale atakapoinamisha kichwa chake, itaonekana kama matonetone ya maji yanadondoka kutoka kichwani kwake na atakapoinuwa kichwa chake itaonekana kama vile lulu inadondoka kwa sura ya matone. Kafiri yeyote atakayefikiwa na pumzi yake ambapo pumzi hiyo itafika masafa ya mbali na upeo wa jicho lake- hatonusurika na kifo. Baadae mwana wa Mariyamu atamwinda Dajjal na kumuwahi kwenye lango la Lyadda (Taz.Tanbihi 9) na kumuuwa”. (Muslim, Dhika Dajjal; Abu Dawud, Kitab ul-Malahim, Bab: Khuruj; Dajjal Tirmidhi, Abwab-ul-Fitan; Bab; Fitna al-Dajjal, ibn Majah, Kitab ul-Fitna, Bab; Fitna al-Dajjal).

-Abdullah b. Amr b. al-As kasema kuwa Mtume wa Allah alisema:

“Dajjal atatokeya kwa watu wangu na ataishi kwa arobaini ( hapa mpokeyaji wa Hadith hana hakika kama Mtume alitaja siku arobaini, miyezi arobaini au miyaka arobaini). Kisha Allah atamtuma Isa, mwana wa Mariyamu duniyani. Kwa wajihi atafanana na “Urwa b. Masud (swahaba wa Mtume). Isa atamwinda dajjal na kumuuwa. Kufuwatiya hili, kwa kipindi cha miyaka saba hali ya mambo duniyani itakuwa kwamba ugomvi baina ya watu wawili hautaonekana”

(Muslim, Dhikr-ul-Dajjal).

Hudhaifa b. Usaid al-Ghifari anasema kuwa “pale Mtume mtukufu alipotutembeleya wakati tulipokaa kundi na kuongeya, Mtume akauliza, Mnasemeshana nini: “Kiyama hakitasimama kabla ya kuonekana ishara kumi. Kisha akazitaja ishara hizo:

-Moshi

-Dajjal

-Daabba

-Juwa kuchomoza upande wa magharibi

-Kushuka kwa Isa mwana wa Mariyamu(as)

-Kutokeya kwa Yaajuj na Maajuja

-Miporomoko mitatu mikubwa ya ardhi, mmoja upande wa mashariki

-Wa pili upande wa magharibi

-Na wa tatu katika visiwa vya Arabuni

-Mwishowe,Moto mkubwa utakaozuka Yemen utakaowaswaga watu kwenye uwanja wa mkusanyiko wa siku ya Kiyama.

(Muslim, Kitab ul-Fitan wa Ashtrat-us Sa’h: Abu Dawud, Kitab ul-Malahim, bab; Amarat ul-Sa’h)

Imeripotiwa na Thauban Mtumwa aliyepewa uhuru na Mtume kuwa Mtume (saw) alisema: “MwenyeziMungu atayakinga makundi mawili ya Umma wangu na moto wa Jahanamu. Kundi moja ni la wale watakaoivamiya India; na lingine ni la wale watakaojiunga na Isa mwana wa Mariyamu (as). (Nasa’i, Kitab ul-jihad; Musnad Ahmad, Bisilsila Riwayat Thauban).

Mujamme b. jariya Ansari amesema: “nilimsikiya Mtume mtukufu akisema: Isa mwana wa Mariyamu atamuuwa Dajjal kwenye lango la Lyadda.” (Musnad Ahmad, Tirmidhi, Abwab- ul-Fitan).

Abu Umama al-Bahli (akimuelezeya Dajjal katika hadith ndefu) amesema, “Muda ule ule Imamu wa Waislamu atakaposimama mbele kusalisha sala ya alfajiri, Isa mwana wa Mariyamu atashuka miyongoni mwao. Imamu atarudi nyuma kumpa nafasi Isa asalishe. Lakini Isa huku akimpigapiga Imamu huyo mabegani atasema: “Hapana wewendiye utakayesalisha kwani jamaa hii imekusanyika kukufuwata wewe.” Hivyo Imamu huyo atasalisha. Baada ya sala kwisha Isa (as) ataamuru; “funguweni Lango”, lango litafunguliwa.

Dajjal atakuwepo nje ya lango hilo na kikosi cha askari elfu sabini wa Kiyahudi. Mara tu Dajjal akimuona Isa (as) atamwambiya: “nitakushambuliya kwa nguvu kiyasi kwamba hutaweza kunusurika”. Isa atamwinda na kumuwahi kwenye lango la mashariki ya mji wa Lyadda. Mungu atafanya Mayahudi kushindwa. Duniya itajaa Waislamu kama vile mtungi ujaavyo maji hadi kwenye mfuniko. Duniya nzima itatamka kalima moja na ibada itafanywa kwa ajili ya Allah (Ibn majah,” Kitab-ul-Fitan: Bab: Fitan Dajjal).

Uthman b. Abi al- As ameripoti kuwa alimsikiya Mtume wa Allah akisema: “Na Isa mwana wa Mariyamu atashuka wakati wa sala ya Alfajiri. Imamu wa Waislamu atamwambiya, “Ewe roho wa Mungu, uwe Imamu wetu.” Atajibu, Watu wa umma

huu ni viongozi wao kwa wao.” Hapo Imamu wa Waislamu atasogeya mbele na kuongoza sala. Baada ya sala kwisha Isa atashika silaha yake na kumsogeleya Dajjal. Dajjal,akimuwona Isa tu ataanza kuyeyuka kama risasi. Isa atamuuwa kwa silaha yake. Washirikai wa dajjal watashindwa. Watatimuwa mbiyo. Lakini hawatapata pa kujificha. Hata miti nayo itapiga kelele. “ Enyi wachaMungu, Kafiri huyu hapa kajificha nyuma yangu.” Mawe nayo yatasema, “Enyi wachaMungu

kafiri huyu hapa kajificha nyuma yangu.” (Musnad Ahmad,Tabarani, Hakim).

Samura b. Jundub (katika Hadith ndefu) anatowa kauli hii iliyosemwa na Mtume: “Basi majira ya asubuhi Isa mwana wa Mariyamu atashuka miongoni mwa Waislamu. Na MwenyeziMungu atafanya dajjal na kikosi chake kushindwa vibaya sana. Hata kuta na mizizi ya miti itapiga kelele, “Enyi wachaMungu kafiri huyu hapa anajificha nyuma yangu. Njooni mumshambuliye afe” (Musnad, Ahmad, Hakim).

Hadith iliyopokelewa na na imam b. Husain inasema kuwa Mtume wa Allah kasema: “Daima kutakuwa na kundi la watu miyongoni mwa wafuwasi wangu ambao watashikamana barabara na imani katika haki na watawashinda kabisa maadui zao hadi Allah atowe amri na Isa mwana wa Mariyamu (as) ashuke duniyani” (Musnad Ahmad).

-Kwa mnasaba wa kisa wa Dajjal, Bi Aisha (ra) karipoti kuwa “Sayidina Isa (as) atashuka na kumuuwa Dajjal. Baada ya hapo Isa (as) atatawala duniyani kama kiongozi mwadilifu na Mtawala mkarimu kwa miyaka arobaini” (Musnad Ahmad).

-Safina, mtumwa aliyepewa uhuru na Mtume wa Allah kasema (kuhusiyana na kisa cha Dajjal) kwamba “Sayidina Isa (as) atashuka na Mungu atayamaliza maisha ya Dajjal jirani na kiteremko cho Afiq” (Taz.Tanbihi 10). (Musnad Ahmad).

-Sayidina Hudhaifa al Yama amesimuliya (kuhusu Dajjal), “Pale Waislamu watakapounga safa kusali, Isa mwana wa Mariyamu atashuka kutoka mbinguni mbele ya macho yao. Pale sala itakapokwisha atawaambiya watu: “wekeni njiya wazi baina yangu na adui huyu wa Mungu”. Mungu atawapa ushindi Waislamu dhidi ya majeshi ya Dajjal. Waislamu watawaadhibu maadui kwa adhabu kali. Hata miti na mawe nayo yatapiga kelele, “Ewe mja wa Allah, ewe mja wa Rahman, ewe Muislamu, njoo Yahudi huyu hapa kajicha nyuma yangu, muuwe”. Kwa njiya hii Mungu atafanya Wayahudi waangamizwe na Waislamu ndio watakaotakaoshinda. Watavunja msalaba, watauwa nguruwe na kufuta jiziya (kodi watozwayo wasioWaislamu).” Mustadrak Hakim- tafsiri fupi ya Hadith hii imeandikwa katika Muslim. Hafiz Ibn Hajar katika Fath-ul-Bari, Juz. VI, uk. 450 ameithibitisha Hadith hii kuwa ni sahihi)

Hizo zilizonukuliwa juu ni jumla ya Hadith ishirini na moja, ambazo zimesambazwa kwa mapokeo ya Maswahaba kumi na wanne wa Mtume mtukufu na zimenukuliwa kwa marejeleo sahihi katika vitabu sahihi zaidi vya Hadith. Isitoshe kuna Hadith nyingine chungu tele zinazozungumziya suwala hilohilo lakini hatukuzionesha hapa kwa sababu ya uchache wa nafasi. Tumezichukuliya kama mfano zile Hadith ambazo ni madhubuti na sahihi kwa ule mlolongo wake wa upokezi.

 

Hukumu ya Hadith hizi

Mtu yeyote anayesoma Hadith hizo atafikiya hitimisho kuwa hazitaji ujiyo wa Masihi aliyeahidiwa wala Masihi wa mfano au taswira ya masihi. Maneno yaliyonukuliwa hapo juu hayakuwacha mwanya kwa mtu yeyote aliyezaliwa kutokana na tone la manii katika tumbo la uzazi kujitangaza, “mimi ni yule Masihi ambaye ujiyo wake ulibashiriwa na Mtume Muhammad.”

Hadith zote hizo zinathibitisha waziwazi na kwa usahihi kuwa kushuka kwa Isa mtukufu ambaye alizaliwa na Mariyamu bila ya nyenzo ya baba miyaka elfu mbili iliyopita. Kwa kweli hapa hakuna faida ya kufunguwa mdahalo wa ama Isa Mtukufu kafa au yuhai akiwa sehemu fulani hapa ulimwenguni.

Jaaliya amekufa, Mungu anao uweza wa kumuhuisha (Taz.Tanbihi 11), vinginevyo si jambo lililo nje ya uweza wa Mungu kumuweka hai mtu sehemu fulani ulimwenguni kwa maelfu ya miyaka; na kumrudisha mtu duniyani kwa idhini yake. Kwa kiwango chochote Muumini, kwa ukweli na utukufu wa Hadith hizo, hatakuwa na shaka kuwa Hadith hizo zilibashiri ujiyo wa “Isa mwana wa Mariyamu na si mwingine yeyote yule.

Kinyume chake kama mtu hana imani na Hadith hizi, hatakuwa mtu wa kuamini ujiyo wa yeyote yule kwani Hadith ndio msingi pekee wa imani juu ya ujiyo huwo. Kutokana na haya yote ni hoja ya ajabu na ya kipuuzi kuichukuwa imani juu ya ujiyo wa Isa itokanayo na hadith na kuiondowa katika mnasaba wake wa wazi na Isa, mwana wa Mariyamu ili kumpachika “Isa mpya wa mfano” mahala pa mwana wa Mariyamu.

Nukta nyingine inayodhihirishwa na Hadith hizi ni kuwa Isa wa Mariyamu hatashuka tena katika nafasi ya Mtume mpya aliyeteuliwa na Mungu. Hatapokeya wahayi kutoka kwa Mungu.

Hataleta ujumbe wowote mpya au kuleta sheriya mpya kutoka kwa Mungu wala hatorekebisha au kuongeza au kupunguza shariya ya Muhammad. Wala Isa mwana wa Mariyamu hataletwa ulimwenguni kuja kubadilisha imani. Isa mwana wa Mariyamu hatawalinganiya watu wauamini utume wake wala hataanzisha jamii ya wafuwasi wapya (Taz. Tanbihi 12).

Atateuliwa kukamilisha kazi fulani ya kung’owa fitna ya Dajjal. Ili kutimiza lengo hilo, Isa (as) atashuka kwa namna ambayo wale Waislamu atakaojitokeza miongoni mwao, hawatakuwa na shaka yoyote juu ya haiba yake kuwa yeye ndiye Isa mwana wa Mariyamu ambaye ujiyo wake ndio ule uliobashiriwa na Mtume Muhammad. Isa atajumuika na jamii ya Waislamu na atasali nyuma ya Imamu wa Waislamu (Taz.Tanbihi 13).

Atamruhusu Imamu amtanguliye yeye ili kudhihirisha kuwa yeye hakuja kujitangaza kama Mtume au kufanya kazi ya utume. Hapana shaka kuwa pale anapokuwepo Mtume miongoni mwa jamii ya watu hakuna mtu mwingine anayeweza kuchukuwa nafasi ya uimamu au uongozi.

Ndiyo kusema wakati Isa atakapokuwa miongoni mwa Waislamu, ukweli huu utadhihiri kwa walimwengu kuwa yeye hakuja kuchukuwa nafasi ya utume.

Kwa msingi huu suwala la kufunguwa komeo la utume kwa ujiyo wa pili wa Isa halitahusishwa kabisa. Labda ingeliweza kusemwa (bila kuyalinganisha kikwelikweli mambo haya mawili) kuwa ujiyo wa Isa utakuwa sawa na uteuzi wa Mkuu wa zamani wa nchi kufanya kazi fulani ya dola chini ya utawala wa Kiongozi aliyepo.

Si vigumu kwa mtu mwenye akili ya kawaida tu kuelewa kuwa uteuzi wa kiongozi wa zamani wa nchi kufanya kazi fulani ya dola chini ya utawala uliopo si ukiukaji wa katiba ya nchi.

Isipokuwa mambo haya mawili ndiyo yanayokiyuka sheriya ya nchi: Jambo la kwanza, iwapo kiongozi wa zamani anataka kuchukuwa tena madaraka. Jambo la pili, iwapo mtu huyo ataukana utawala uliopo wa kiongozi aliyetawafu, kwani hii itakuwa sawa na kupinga uhalali wa kazi zilizofanywa na utawala wa awali.

Ukiondowa mambo hayo mawili, uteuzi wa kawaida tu wa Kiongozi wa zamani haubadilishi msimamo wa kikatiba. Hivyo ndivyo ulivyo ujiyo wa pili wa Isa. Hata hivyo, kama akichukuwa tena madaraka ya utume kuanza kufanya kazi ya utume au kinyume na hivyo mtu akiukataa utukufu wa Isa kama Mtume wa zamani, mambo yote haya mawili yanaleta ukiukaji wa sheriya ya Mungu.

Kwa upande mmoja Hadith hizi zinathibisha kuwa hakuna Mtume atakayekuja baada ya Muhammad. Wakati huo huo Hadith hizo zinabashiri ujiyo wa pili wa Isa mwana wa Maryamu. Hii inatosha kudhihirisha kuwa wakati wa ujiyo wa pili wa Isa ulimwenguni Isa hatafanya kazi za utume.

Kwa namna hiyohiyo, kuja kwake hakutazusha suwala la imani mpya au suwala la kuritadi miongoni mwa wafuwasi wa Uislamu. Yeyote anayeikataa imani kuwa Isa ni nabii wa zamani, huyo ni Murtadi.

Mtume mtukufu mwenyewe aliuthibitisha utakatifu wa Isa kama Nabii aliyetanguliya. Hivyo. Wafuwasi wa Muhammad, tangiya mwanzo, daima wameuwamini utakatifu wa Isa kama Nabii. Imani hii itadumu hivyo hivyo hata pale atakapokuja tena.

Watadumisha imani yao juu ya utakatifu wa Isa kama Nabii aliyetanguliya. Imani hii haipingani na ukomo wa unabii kwa Muhammad wala haidhihaki imani juu ya ujiyo wa pili wa Isa ulimwenguni.

Nukta ya mwisho inayowekwa wazi na Hadith hizi na nyinginezo ni ile ihusiyanayo na ukweli kuwa Dajjal ( ambaye ili kukomesha maovu yake makubwa Mungu atamtuma Isa mwana wa Maryamu (as), atatokeya miongoni mwa jamii ya Wayahudi na kwamba atajinadi kuwa yeye ndiye “Masihi.”

Hakuna mtu anayeweza kuuelewa undani wa ukweli huu bila kuisoma historiya ya Wayahudi na imani zao. Baada ya Sayidina Suleiman (as), Bani Israili walipata udhalili juu ya udhalili hadi wakawa watumwa wa falme za Babil na Assiriya na mabwana zao mabeberu wakawatawanya huku na kule ardhini.

Katika wakati huo wa historiya yao, nabii wa Wayahudi akaanza kutowa habari njema za kuja kwa “Masihi.” kutoka kwa Mungu ambaye atawakombowa kutoka katika udhalili.

Kwa kuzingatiya bishara hizo Wayahudi kwa muda mrefu walimsubiri “Masihi” ambaye angekuwa mfalme. Mfalme huyo angepambana na kutwaa nchi. Angewakusanya wayahudi kutoka duniyani kote na kuwakutanisha Palestina.

Angeunda Utawala mkubwa wa Wayahudi. Kinyume na matarajiyo yao makubwa, pale Masihi aliyeteuliwa na Mungu Isa mwana wa Maryamu alipokuja bila jeshi la kutwaa nchi, Mayahudi wakaukataa unabii wake na wakadhamiriya kuutowesha uhai wake.

Tangiya wakati huo Mayahudi ulimwenguni kote wakawa wanamsubiri “Masih Mau’ud”, “Masihi aliyeahidiwa” ambaye habari zake njema zilibashiriwa na Manabii wao wa zamani. Vitabu vyote vimejaa njozi njema za wakati huo wa furaha. Wayahudi kwa karne nyingi wamekuwa na furaha hii ya ndotoni inayotokana na maelezo ya wakati huo katika Talmud na katika maandiko ya marabi.

Jamii ya Wayahudi imedumisha matumaini kuwa “Masihi huyu aliyeahidiwa” atakuwa Jemedari mkubwa wa kijeshi na kiongozi mkubwa kisiyasa. Atawarudishiya tena nchi yao baina ya mto nile na Euphrates (ambayo wayahudi mara zote wameyatazama kama urithi wao wa kiumeni). Atawakusanya wayahudi kutoka sehemu zote ulimwenguni na kuwakutanisha tena katika nchi hii.

Leo hii tunapoiangaliya hali ya mambo Mashariki ya Kati kwa mtazamo wa bishara za Mtume Mahammad, mara moja tunaona kuwa mazingira yamekwishaandaliwa kwa ajili ya kuibuka kwa Dajjal ambaye alikwishabashiriwa na Mtume mtukufu, Dajjal huyo atajitokeza kama “masihi mtarajiwa” wa Wayahudi.

Waislamu wametimuliwa katika sehemu kubwa ya Palestina ambapo huko Dola ya Wayahudi iitwayo “Israil” imesimamishwa. Wayahudi kutoka sehemu zote za duniya wanamiminika huko. Amerika, Uingereza na Ufaransa zimesaidiya kuifanya dola hii iwe na nguvu za kutisha za kijeshi.

Wanasayansi na wanatekinolojiya wanaiendeleza nchi hii kwa kasi kwa msaada mkubwa wa makao makuu ya Wayahudi. Nguvu za kijeshi na kitekinolojiya za Israil zinaweka tishiyo kubwa kwa nchi jirani za Waislamu. Viongozi wa Israil bado hawajachana kabisa na hila zao za kuikombowa “nchi ya urithi wao wa kuumeni.”

Ramani ya Dola ya usoni ya Israil ambayo wamekuwa wakiichapisha kwa muda mrefu inaonesha kuwa wanataka kuijumuisha Syriya, Lebanon, Jordan na takriban eneo lote la Iraq mbali na kuchota Askandron Uturuki, Sinai na eneo la Delta kutoka Misri, Maeneo ya Hijaz juu na Najid kutoka Saudi Arabiya.

Hii bila shaka inajumuisha piya Mji mtakatifu wa Madina. Katika mazingira haya ni dhahiri kabisa kuwa kwa kutumiya fursa ya hali ngumu iliyosababishwa na Vita ya Duniya, kwa hakika, Wayahudi watafanya hila kuyanyakuwa maeneo haya.

Ndipo hapo atakapotokeya dajjal ambaye Wayahudi watamuwona kama ndiye “Masihi aliyeahidiwa”. Mtume mtukufu siyo tu alibashiri kuja kwa Dajjal bali piya aliwatahadharisha Waislamu kuwa watapata shida kubwa na kwamba siku moja ya mateso itaonekana kama mwaka mmoja wa mateso na dhahama.

Ni kwa sababu hii ndiyo maana Mtume wa Allah alikuwa akiomba ulinzi dhidi ya shari (fitina) kubwa ya Masihi Dajjal na alikuwa akiwahimiza maswahaba wake kumuomba Allah awanusuru na shari ya zama hizo mbaya.

Ni jambo la hakika kuwa Allah hatamtuma “Isa wa mfano,” Atamtuma Isa yuleyule aliyezaliwa na Maryamu na ambaye wayahudi walikataa kumtambuwa kama mtume miyaka elfu mbili iliyopita.

Atamtuma Isa yuleyule ambaye Wayahudi waliamini kuwa walimuondowa kwa kumsulubu. Mahali halisi atakaposhukiya Isa siyo Indiya, Afrika au Amerika.

 

Ni Damascus ambako kuna umbali wa karibu maili 50-60 kutoka mipaka ya Israili. Ukikumbuka maneno ya Hadith tuliyoinukuu hapo juu, utaona kuwa si vigumu kuelewa kuwa Dajjal atajipenyeza Syria na kikosi cha Wayahudi 70,000, na watasimama mbele ya Damascus. Katika kipindi hicho cha tafrani, Isa mwana wa Maryamu atashuka jirani na Mnara mweupe katika eneo la mashariki ya Damascus.

Baada ya sala ya Alfajiri, Isa atasonga mbele na Waislamu kwa ajili ya kupambana na Dajjal. Adui atarudi nyuma kabla ya shambulio la nguvu la Isa mwana wa Maryamu ambapo Dajjal atakimbiliya Israili kupitiya njiya ya kiteremko cha Afiq. (Rejeleya Hadith Na 21). Isa (as) atamwinda Dajjal na kummaliza kwenye uwanja wa ndege wa Lyadda (Hadith Na 10-14,15).

Mauwaji makubwa ya Wayahudi yatatokeya ambapo kila mmoja waoataangamiya. Taifa la Wayahudi litatokomezwa. (Hadith 9-15-21).

Kwa ukweli utakaohubiriwa na Isa, dini ya ukristo itatoweka (Hadith Na 1-2-4-6). Na wafuwasi wa dini zote, baada ya kule kukataa kwao zamani, wataungana kuunda undugu mmoja na wa pekee wa Uislamu. Hadith zinaubainisha ukweli huu waziwazi bila shaka yoyote.

Kutokana na hayo yote hapo juu mtandao wa propaganda ambao umewekwa nchini mwetu (Na jumuiya ya Ahmadiya/Qadiyani) kwa jina la Masih Mau’ud, “Masihi aliyeahidiwa” bila shaka ni batili na ni mkakati wa upotoshaji.

Moja kati ya mambo ya kuchekesha ya jumuiya hii ni kuwa Mirza ghulam Ahmad Qadiani ambaye anajiona ndiye mlengwa wa bishara za Sayidina Muhammad ametowa ufafanuzi wa ajabu wa utambulisho wake kama “Isa mwana wa Maryamu”.

“Yeye (Mungu)alinipa jina la Maryamu katika sura ya tatu ya Barah-ini- Ahmadia. Baada ya hapo kama inavyodhihirika katika Barahin-i-Ahmadia nikalelewa kwa sura ya Maryamu kwa miyaka miwili. Kisha mwili wangu ukajazwa roho ya Isa kama vile mwili wa Mariyamu ulivyojazwa roho ya Isa na kwa maana ya kitamathali nikawa mjamzito kwa roho ya Isa. Mwishowe baada ya kipindi cha miezi mingi (zaidi ya miezi kumi), nikageuzwa kutoka Maryamu kuwa Isa kwa ufunuo wa Mungu, ambao umeandikwa mwishoni mwa sura ya nne ya Barahin-i-Ahmadia. Hivyo kwa njiya hii nikawa mwana wa Maryamu”. (Kashti-e-Noah, 87-89).

Kwa maneno mengine kwanza Mirza alikuwa Maryamu, kisha akapata mimba na mwishowe kutoka katika tumbo lake mwenyewe akatokeya kama Isa mwana wa Maryamu. Hata hivyo, kulikuwa na kikwazo kimoja kilichobakiya.

Kwa mujibu wa Hadith, Isa mwana wa Maryamu atatokeya Damascus,mji mashuhuri wa Syria ambao umevuma kwa miyaka elfu kadhaa, hadi leo mji unajulikana kwa jina hili katika ramani ya duniya.

Utata huu ukafafanuliwa na maelezo mengine ya kuchekesha: “Ifahamike kuwa kwa ajili ya ufafanuzi wa neno “Damascus.” MwenyeziMungu amenifafanuliya kwa ufunuo kuwa Hapa jina hilo hilo Damascus limetolewa kwa kijiji ambacho wakazi wake wana sifa za Yazid na ni wafuwasi wa tabiya na mawazo ya Yazid chafu. Mji huu wa Qadian, kwa sababu kuwa wengi wa wakazi wake wana sifa za Yazid kwa tabiya zao, unanasibiyana na una haiba fulani inayofanana na Damascus (Marginal note of Izala-i-Auhma, uk. 63-73).

Lakini hivyo sivyo kabisa, lipo tatizo jingine tena linalohitaji ufafanuzi nalo ni kwamba Hadith zimebashiri kuwa Isa atashuka jirani na Nguzo nyeupe. Tatizo lilitatuliwa pale “Isa mpya” alipojengewa nguzo yenye rangi nyeupe.

Hadith zimetaja kuwa nguzo hiyo nyeupe itasimama kabla ya kushuka kwa Isa jirani nayo lakini kule Qadiani nguzo ilijengwa baada ya kutokeya kwa “Masih Mau’ud. Lakini achiliya mbali tofauti hii. Yeyote asomaye fafanuzi hizo za “Masih Mau’ud” kwa macho safi atafikiya hitimisho kuwa huu ni upotoshaji unapenyezwa waziwazi na mzushi huyu.

Tanbihi

Tanbihi 1

 

Kwa nukta hii wale wanaoukanusha mwisho wa Utume wa Muhammad hutaka kuijuwa Hadith ambayo dai hili limeripotiwa.Swali hili kwa kweli linadhihirisha umbumbumbu wao.Qur’an inatowa majibu ya madai haya ya Mafatani kwa nukta kadhaa bila kulitaja dai lenyewe.Hata hivyo katika kila jibu kila aya husika inatowa ushahidi sahihi juu ya dai linalojibiwa. Kuhusiyana na suwala hili piya jawabu lina sehemu ya swali. Utumizi wa kiunganishi “bali”mwishoni mwa sentensi unaashiriya sehemu ya swali bado haijajibiwa.Hivyo, sentensi ya pili ndiyo inayotowa jibu la sehemu iliyobaki ya swali hilo. Sentensi ya kwanza iliwabainishiya wapinzani jawabu la swali lao kuwa eti “Muhammad alimuowa mkwewe”. Hata hivyo nukta ya pili ya swali kuwa wapi ilitoka shurti kwa Mtume kufanya hivyo bado nayo ilihitaji jibu piya. Jibu hilo likatolewa na sentensi iliyofuwata katika aya hiyo.

 

"Lakini, kwa hakika Muhammad ni Mtume wa MwenyeziMungu na ni Mwisho wa Mitume wa Mungu"

 

Nukta hii yaweza kufafanuliwa zaidi kwa kuchukuliya mfano wa mazungumzo ya kawaida. Mtu anaweza kusema, “Zaid hakuinuka bali Bakari ndiye aliyesimama wima”. Hapo hii inaleta maana kuwa Zaid hakuinuka lakini hii haishii hapo, kwani inazusha swali. Kama Zaid hakuinuka nani basi aliyesimama? “ kifungu cha maneno, bali Bakari ndiye aliyesimama wima ndicho kinachotowa majibu ya swali. Ni vivyo hivyo katika jibu la swali la hilo.

Tanbihi 2

Tumezirejeleya kamusi tatu hapa lakini bado ufafanuzi wa suwala hili hauishii katika makamusi haya tu. Kamusi zote sanifu za lugha ya Kiarabu zinalitafsiri neno Khatam kwa maana hiyo tuliyoitowa. Lakini wale wanaokanusha mwisho wa utume katika jitahada zao za kufanya shambulio la kinyemela dhidi ya dini ya MwenyeziMungu wanadai kuwa kama tutamuelezeleya mtu fulani kama “Mwisho wa Washairi” au “Mwisho wa Wanasheriya” au “Mwisho wa Wafasiri”, si lazima kwamba tuwe na maana kuwa hakuna mshairi au mwanasheriya au mfasiri atakayekuja baada yao, bali tunamaana kuwa sifa zote za utendaji wao zimejikita kwa watu hao. Hata hivyo, maana halisi ni kuwa pale tunapotumiya mifano hii ya kummwagiya sifa mtu fulani bado hatubadilishi au kuondosha maana halisi ya neno “Mwisho”. Ni makosa kudhani kuwa kwa matumizi ya kitamathali yanayoelezeya sifa au ubora wa mtu, ndiyo basi neno “Mwisho” linapotyeza maana yake halisi au maana yake ya asili ambayo ni “hatima”. Dhana kama hiyo yaweza tu kukubalika kwa mtu asiyekuwa na elimu ya msingi ya kanuni za sarufi. Hakuna kanuni ya kisarufi katika lugha yoyote ambapo kwayo maana ya kitamathali ya neno yaweza kuchukuliwa kama maana halisi. Isitoshe, maana ya kitamathali habadilishi au kufuta maana halisi ya neno.

Unapomwambiya Mwarabu, “Ja Khatam ul-Quum” kwa hakika hataichukuliya kauli hii kwa maana ya mtu mtu bora mwenye sifa kubwa katika kabila amekuja. Bali kinyume chake atamaanisha kuwa kabila zima hadi mtu wa mwisho kabisa limekuja.”

Hakuna hoja tena ya kutafakari. Misemo hiyo kama “Mshairi wa Mwisho,” Mwanasheriya wa Mwisho au “ “Msimulizi wa Mwisho wa hadith” ni sifa zinazotumiwa na binadamu kuwasifu wanadamu wenzao ambao wanawaona ni bora na wenye sifa bora.

Wale wanaotumiya misemo hii ya kusifu watu, kwa kweli hawawezi kusema wala kujuwa kuwa watu wenye sifa kama hizo watakuja huko mbele au la. Kwa hiyo kwa wanadamu misemo hii ni ya kutiya chumvi, lakini Mungu anapotumiya sifa fulani imeishiya kwa mtu huyo hakuna sababu ya kuichukuliya kwa maana ya kitamathali kwa usemi wa kibinadamu.. Kama Mungu angemtangaza mtu fulani kuwa ni “Mshairi wa Mwisho”basi kweli mtu huyo angekuwa Mshairi wa mwisho kwa maana ya kiistilahi ya neno hilo. Kama mtu anamteuwa mtu fulani kama mtume wake wa “Mwisho”, hakuna tena uwezekano kwa mtu mwingine yeyote kupata hadhi hiyo baada yake.

Mungu ni Mjuzi wa mambo yote. Lakini binadamu hana isipokuwa elimu ndogo tu. Ikiwa hivyo basi, mtu anawezaje kumaanisha sifa ya mtu kuwa “Mshairi wa mwisho” au “Mwisho wa washairi wote” kwa maana ileile kama Mungu anavyomtangaza mtu kuwa “Mtume wa Mwisho” ?

Tanbihi 3

Wakirejeleya Hadith hii wale wasioamini Mwisho wa utume hudai kuwa Mtume Mtukufu (saw) aliuita msikiti kuwa ni msikiti wa mwisho licha ya ukweli kwamba huo siyo msikiti wa mwisho kwani misikiti chungu tele imejengwa baada ya msikiti huwo duniyani kote. Vivyo hivyo pale mtume mtukufu aliposema: “Mimi ni Mtume wa Mwisho”, haikuwa na maana kuwa mlolongo wa Mitume umekoma, bali Muhammad alikuwa wa mwisho kwa mnasaba wa ubora wake miongoni mwa Mitume wa Mwenyezimungu ambapo hata msikiti wake ulikuwa wa mwisho kwa maana hiyo hiyo. Hoja hiyo ya kipuuzi ni ushahidi usiopingika wa ukweli kuwa watu hawa wamepoteza ule uwezo wa kuelewa maana sahihi ya maneno ya MwenyeziMungu na yale ya Mtuime wake. Hata mtazamo wa juujuu tu kwa njiya ya isinadi ya Hadithi ambazo kwa muktadha wake Hadith hii mahususi imenakiliwa unatowa maana sahihi ya maneno ya Mtume Mtukufu yaliyo wazi kwa mtu yeyote. Kwa muktadha huu Hadith mbalimbali ambazo Imamu Muslim amezikariri kutoka kwa Sayidina Abu Huraira, Sayidina “Abdullah bin” Uma na mama wa waumini bi Maimuna zinasema kuwa kuna misikiti mitatu tu duniyani ambayo inatukuzwa kwa utukufu mkubwa ambapo misikiti hii ndiyo mitukufu zaidi ya misikiti yote. Ibada katika misikiti hii huwa na thawabu kubwa mara elfu kulinganisha na sala inayosaliwa katika misikiti mingine. Ni kwa sababu hii kwamba imehimizwa kisheriya kufunga safari kwenda kusali katika misikiti hii. Hakuna msikiti mwingine wowote ukiondowa hii mitatu, unaoweza kudai utukufu huwo kuwa mtu afunge safari kwenda kusalia huku akiiacha misikiti mingine yote. Miongoni mwa misikiti misikiti mitatu yenye utukufu mkubwa katika Uislamu ni hii; wa kwanza ni Masjid Al-Haram ambao ulijengwa na Nabii Ibrahim (as), wa pili ni “Masjid al-Aqsa” ambao ulijengwa na Nabii Suleiman (as); na wa tatu ni “Masjid-I-Nabawi” mjini madina ambao uliasisiwa na Mtume Muhammad (saw). Maneno ya Mtume mtukufu kuhusiyana na “msikiti wa mwisho” yatazamwe kwa muktadha huu. Maneno ya Mtume yalikuwa na maana kuwa Hakuna Mtume atakayekuja baada yake hivyo hakutakuwa na Msikiti wa nne baada ya Masjid-I-Nabawi (Msikiti wa Mtume wa mwisho).Hivyo, kinachokuja hapa ni kuwa hakuna msikiti mwingine unaopaswa kupata utukufu huo, eti kwamba katika Msikiti ibada ilipwe thawabu nyingi zaidi kulinganisha na misikiti mingine na zaidi ya hivyo hakutakuwa na msikiti wa nne ambao watu, kisheriya au kwa kutaka, watalazimika kufunga safari ili kwenda kusaliya humo.

Tanbihi 4

Kinyume na maneno ya Mtume Mtukufu, wale wanaokanusha Mwisho wa Utume hunukuu maneno yafuwatayo yanayodaiwa kusemwa na Bi Aisha: “Sema, kwa hakika, Mtume Mtukufu ndiye Mtume wa Mwisho wa MwenyeziMungu; lakini usiseme kuwa hakuna mtume atakayekuja baada yake” Kwanza kabisa ni ujasiri wa ajabu kunukuu maneno ya Bi Aisha kupinga hukumu ya wazi ya Mtume. Isitoshe maneno hayo yanayosemekana kusemwa na Bi Aisha hayana uthibitisho. Hakuna kitabu chochote cha Hadith sahihi chenye maneno haya ya Bi Aisha. Wala hakuna mkusanyaji yoyote mashuhuri wa Hadith aliyerekodi au kuirejeleya kauli hiyo. Hadith hii imetolewa katika Tafsiri iitwayo Durr-Manthur na kitabu cha Hadith kijulikanacho kama Takmilah Majma-ul-Bihar, lakini chanzo na ithibati yake havijulikani. Ni kiwango cha juu cha ujasiri kutowa kauli ya Sahaba huyu wa kike wa Mtume ili kuyapinga maneno ya wazi ya Mtume Mtukufu ambayo Muhadithuna mashuhuri wameyasambaza kwa isinadi sahihi.

Tanbihi 5

“Maana ya kuvunja Msalaba” na “Kuuwa nguruwe” ni kuwa Ukristo utafutika. Msingi wa dini ya Ukristo unatokana na imani kuwa Mungu alimsulubisha Mwanawe wa pekee (Nabii Isa as) msalabani na kumfanya afe kifo cha “laana” ili aweze kufidiya dhambi za mwanadamu. Miongoni mwa wafuwasi wa Mitume, Wakristo wao wamejiweka peke yao kwa kuikataa shariya yote ya Mungu na kuishikiliya imani hii tu. Nguruwe aliharamishwa na Mitume wote lakini Wakristo wao wameendeleya tu kuihalalisha.Hivyo, pale Isa (as) atakapotokeya na kutangaza, “Mimi si mwana mwana wa Mungu; Sikufiya msalabani wala sikufuta dhambi za mtu yeyote”, msingi mzima wa imani ya Kikristo hapo utakuwa umebomoka. Vivyo hivyo sifa nyingine pekee ya Wakristo nayo itafutika pale Isa (as) atakaposema; “Sikupata kuhalalisha nguruwe hata kidogo kwa Wafuwasi wangu wala sikuwaweka huru na mipaka ya Shariya ya Mungu”.

Tanbihi 6

Kwa maneno mengine kauli hii ina maana kuwa tofauti kati ya wafuwasi wa dini mbalimbali itafutika na walimwengu wote wataunga undugu wa Kiislamu. Kwa hali hiyo hakutakuwa na sababu tena ya kumtoza kodi ya kidini mtu yeyote. Ufafanuzi huu unaungwa na na Hadith Na 5 na 15.

Tanbihi 7

Maana yake ni kwamba Isa (as) hatakuwa Imamu wa sala. Atasali nyuma ya Imamu aliyepo wa Waislamu.

Tanbihi 8

Maana ya maneno haya ya Isa (as) ni kuwa, “Mtu yeyote miongoni mwenu awe kiongozi wenu.”

Tanbihi 9

Tafadhali zingatiya kuwa Lod (sasa hivi Lyadda) ipo umbali wa maili chache kutoka Tel Aviv, mji mkuu wa dola ya Israili ndani ya Palestina. Wayahudi wamejenga kituwo kikubwa cha anga katika sehemu hii.

Tanbihi 10

Afiq ambayo siku hizi inajulikana kama Fiq ni mji wa Syria uliopo mpakani baina ya Syria na Israil. Kuna ziwa linaloitwa Tabriya maili chache upnde wa magharibi wa mji huo. Ziwa hili ndiyo chanzo cha mto Jordan, upande wa kusini-magharibi wa ziwa hili kuna njiya inayopita katikati ya milima ambayo inateremkiya umbali wa futi elfu mbili hadi katika Ziwa la Tibriya ambako mto unatokeya. Njiya hii ya mlimani inaitwa Kiteremko cha Afiq (the slope of Afiq).

Tanbihi 11

Wale wakanushao uwezekano huu wapitiye aya ya 250 ya Surati Baqara ambapo MwenyeziMungu anasema kwa maneno ya wazi kuwa alimfisha mmoja wa viumbe vyake kwa miyaka miya moja na baada ya muda huo akamfufuwa.

Tanbihi 12

Maumaa wa Kiislamu wamelifafanuwa suwala hili kwa kina. Allama Taftazani (722 A.H. – 792 A.H.) katika Shara “Aqaid-I-Nasafi kaandika: “Imethibitika kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwisho... Inaposemwa kuwa kwa mujibu wa Hadith kushuka kwa Isa (as) kutatokeya baada ya Mtume Muhammad sisi tutasema hivi: “Naam, jambo hili limeelezwa katika Hadith. Lakini Isa (as) atatokeya kama mfuwasi wa Muhammad. Shariya ya Isa inabaki katika hali ile ile ya kufutika. Ndiyo kusema kuwa yeye hatapokeya ufunuo wowote kutoka kwa Mungu wala hatasimamisha sheriya yoyote. Katika matendo yake yote atamwakilisha Muhammad tu”.

Jambo hilo limesisitizwa na Allama Alusi katika Tafsir Ruh-al-Ma’ani: Hapo baadae isa atakapotokeya, atakuwa na hadhi kama Nabii wa Zamani. Tangu hapo Kwa hakika Mungu hatomuondosheya hadhi yake hii lakini hatafuwata sheriya ya wakati wake kwa sababu sheriya zote ikwemo yake zinabakiya vile vile katika hali ya kufutika. Hivyo itakuwa amri ya Mungu kwa Isa (as) kufuwata kwa maandishi na kwa imani kazi ya kusimamisha sheriya ya sasa ya Muhammad (saw).

Hatapokeya wahai kutoka kwa Mungu wala hatapewa kazi ya kuleta sheriya mpya ya dini. Katika matendo yake yote, Isa ataishi kama mwakilishi wa wafuwasi wa Muhammad na atafanya kazi kama naibu na mmoja wa watawala wa wafuwasi wa Muhammad (saw).

Imam Raz. anaifafanuwa zaidi nukta hiyo kama hivi:Kipindi cha Utume kiliendeleya hadi alipokuja Mtume Muhammad (saw). Pale Muhammad aliponyanyuliwa kuwa Mtume ndipo kipindi cha kuja kwa Mitume kilipofikiya mwisho. Si jambo lisilofahamika kuwa Isa (as) akishuka atakuwa mfuwasi wa Muhammad (saw).

Tanbihi 13

Ingawaje Hadith mbili (Na 5 na21) zina ushahidi wa kutosha kuwa Isa (as) ataelekeya kuwa kama Imamu katika sala kwanza baada ya kushuka kwake, Hadith chungu mzima ambazo ni sahihi zaidi (pitiya Na3,7,9’15,16) zinauzungumziya ukweli kuwa Isa (as) atakataa kusalisha. Atamtaka Imamu aliyepo kupita mbele na kusalisha. Wanazuwoni wote wa Hadith na Mufasiruna wanakubaliyana juu ya jambo hili.

تاريخ الاضافة: 26-11-2009
طباعة